31 Agosti 2020 - 15:22
Ismail Haniya: Azma ya muqawama Palestina ni kuhitimisha mzingiro dhidi ya Gaza

Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa, azama na irada ya taifa na muqawama wa Palestina ni kufanya hima kwa ajili ya kuhitimisha mzingiro wa kidhulma unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Ismail Haniya amesema hayo na kutangaza kuwa, viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) wanafanya hima na juhudi ili kulikwamua eneo la Ukanda wa Gaza na athari za kimaafa zinazosababishwa na mzingiro dhidi ya eneo hilo.

Kiongozi huyo wa Hamas amemtaka Nikolai Miladinov, mjumbe maalumu wa amani wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Asia Magharibi pamoja na asasi hiyo ya kimataifa kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika kuwaunga mkono wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Aidha Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS)  amezitaka nchi za Kiislamu ziliunge mkono ene la Gaza, Quds na taifa zima la Palestina linalokabiliwa na taabu na masaibu mengi kutokana na siasa za ukandamizaji za Israel.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unalizingira eneo la Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2006 wakati Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ilipoibuka na ushindi katika uchaguzi wa Bunge la Palestina. Tangu wakati huo Israel imekuwa ikizuia kuingizwa bidhaa zote muhimu katika eneo hilo kama vile chakula, dawa, vifaa vya ujenzi na kadhalika. 

Hivi sasa wakazi wa Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na mashaka na matatizo makubwa kwa ajili ya kupata huduma muhimu kama dawa, maji na chakula, huku asasi mbalimbali zikitahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea maafa ya kibinadamu katika eneo hilo. 

342/